Women WC 2018 Q: The Falconets kuwasili Septemba 29.

Kikosi cha watu 31 miongoni mwao wapo maofisa 13 wa Timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu kwa wasichana wenye umri wa chini ya miaka 20 ya Nigeria ‘Falconets’ kinatarajiwa kutua nchini usiku wa kumkia Ijumaa Septemba 29, mwaka huu.

Timu hiyo ya wasichana yenye wachezaji 18, watatua Dar es Salaam saa 9.40 (Kwa saa za Afrika Mashariki) usiku na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania, limewapangia kuishi katika Hoteli ya Urban Rose iliyoko katikati ya jiji la Dar es Salaam katika kipindi cha siku tatu watakazokuwa hapa Jijini.

Nigeria wanakuja kucheza na timu ya Taifa ya wasichana wenye umri wa chini ya miaka 20 ya Tanzania ‘The Tanzanite’ kwenye mchezo wa marudiano kuwania kucheza fainali za Kombe la Dunia, Fainali zitakazofanyika Ufaransa hapo mwakani.

Oktoba Mosi. 

Mchezo huo wa marudiano utafanyika Jumapili Oktoba mosi, mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam ulioko Chamazi, Dar es Salaam kuanzia saa 10.00 jioni.

Tanzania ina matumaini ya kufanya vema kwenye mchezo huo wa marudio licha ya kupoteza kwa mabao 3-0 katika mchezo wa kwanza uliofanyika Uwanja wa Samwel Oigemudia ulioko Jimbo la Benin, Nigeria.